Januari 08, 2013
Wanamgambo wa al-Shabaab wanaondoka mfululizo huko Bardhere katika mkoa wa Gedo wakati mamia ya askari wa Somalia, wakisaidiwa na majshi ya Ethiopia, wakisonga mbele kuelekea mjini kudai udhibiti na kurejesha sheria na utaratibu.
Mkazi wa eneo hilo Farhan Mohamed Jama alisema aliiona misafara na magari ya kijeshi ya al-Shabaab yakiondoka kutoka Bardhere kwa muda wa usiku kadhaa, yakienda magharibi kuelekea Burdubo na Dinsor katika mkoa wa Bay.
"Kuna mazingira ya kutokuwepo na sheria mjini na al-Shabaab wametangaza hali ya tahadhari wakijitayarisha na mashambulizi dhidi ya kambi na ngome zake," Jama aliiambia Sabahi. "Katika baadhi ya mitaa na katikati, kuna mamia ya wanamgambo wa waasi ambao wameanza kupiga risasi nzito hewani usiku wa manane wiki hii iliyopita katika jaribio la kuwashitua wakazi na kuonyesha nguvu zao katika eneo hili."
Siku ya Alhamisi jioni (tarehe 3 Januari), al-Shabaab waliwakamata viongozi 13 wa dini na kuwashutumu kuwa wanakula njama za kuvikaribisha vikosi vinavyokaribia, Jama alisema.
Hawa Ahmed Kheyre, muuzaji wa maandazi mwenye umri wa miaka 30 katika soko la Bardhere, alisema kuwa al-Shabaab wamewaondosha baadhi ya wapiganaji wao kutoka mjini ili kujitayarisha kwa vita vya msituni na ulipuaji mabomu.
"Tunaishi katika nyakati za zahama kwa matokeo ya vitisho kutoka kwa watu wenye siasa kali ambao wamezagaa vijijini kote na milimani ya mkoa wa Gedo," alisema. "Tunasumbuliwa na mivutano, mauaji na mashitaka kutoka mikononi mwa wafuasi wa kikundi hiki ambao wamejipenyeza miongoni mwa watu wa eneo hili."
Diyad Abdi Kalil, afisa wa jeshi la Somalia huko Gedo, alisema kwa kweli vikosi vya Somalia vinapanga kuishambulia Bardhere na Burdubo, ambazo bado ziko katika udhibiti wa al-Shabaab, lakini hakusema lini.
"Mkakati wetu wa vita ni kukishinda na kukifukuza kikundi hiki kinachopinga amani kutoka miji na vijiji vinavyovidhibiti kabla ya mwisho wa mwezi wa Januari," Kalil aliiambia Sabahi. "Majeshi yetu yako tayari kuanzisha shambulio na tunasubiri amri kutoka kwa kamanda wetu wa juu na vikosi vyenye silaha. Tutaendelea baada ya kupata amri na tunadhamiria kuanzisha shambulizi la mwisho la kujikinga."
Kuipoteza Bardhere kutakata upatikanaji mahitaji kwa al-Shabaab
Kanali Abbas Ibrahim Gurey, kamanda wa jeshi la Somalia huko Ufurow katika mkoa wa Bay, alisema majeshi kadhaa yanashiriki katika kuulinda mkoa na kuharibu maficho muhimu ya al-Shabaab katika maeneo ya kati na kusini ya nchi, hasa karibu na Bardhere na Burdubo.
Bardhere, wanakoishi watu wengi wa madhehebu ya Sufi, iko katika kingo za mto Shabelle, kilomita 344 kusini magharibi ya Mogadishu. Kwa sababu ya sehemu ilipo katika barabara inayounganisha mikoa ya Bay na Jubba ya Kati, jeshi la Somalia na vikosi vya washirika vinauchukulia mji huu kuwa eneo la mkakati ambalo litazuia uingiaji wa mahitaji muhimu ya wanamgambo wa al-Shabaab.
Vikosi vya washirika vimekuwa vikipanga kuchukua udhibiti wa Bardhere kwa mwaka na nusu sasa. Mwezi Agosti, shambulio la angani kutoka Kenya liliua kiasi cha washukiwa 18 wa wanachama wa al-Shabaab huko Bardhere.
Al-Shabaab walikuwa na kawaida ya kuweka hatua kali za usalama kwa wakazi wa mjini, kama vile amri ya kutotembea usiku na marufuku ya kuuza mirungi, sigara na tumbaku. Wanamgambo pia waliweka vituo vya upekuzi kwenye viunga vya mji.
Raisi wa Somalia arejea juu ya ahadi ya msamaha
Raisi wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alirejea wito wake wa kuwataka wapiganaji wa al-Shabaab kujisalimisha na kutumia fursa ya mpango wa msamaha wa serikali.
"Serikali yangu itapigania amani na tutaanzisha mpango wa kuwarekebisha, kuwapatia mafunzo na miongozo wanamgambo wote watakaoachana na kikundi hicho chenye mafungamano na al-Qaeda," Mohamud aliwaambia waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde tarehe 3 Januari baada ya kurejea kutoka ziari huko Sudani.
"Tutahakikisha fursa za kazi binafsi kwa vijana hawa kama njia ya kumaliza vita hivi na kukusanya silaha haramu ambazo zinaonekana kwa wingi miongoni mwa sehemu nyingi za jamii ya Soamlia," alisema.
Post a Comment